GAVANA WA BENKI KUU TANZANIA AZINDUA SELCOM PESA.
HUDUMA YA KIFEDHA YA KIDIGITALI YENYE MAKATO MADOGO KULIKO.
11 Februari 2025, Dar es Salaam, Tanzania – Katika hafla iliyofanyika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, Benki ya Selcom Microfinance imezindua rasmi huduma yake maridhawa ijulikanayo kama SELCOM PESA, aplikesheni ya huduma za kifedha ambayo imebuniwa mahususi kuboresha namna watanzania wanavyofaidika na huduma za kifedha na kuwapunguzia mzigo wa makato.
Selcom Pesa ni aplikesheni ya huduma za kifedha yenye nia ya kuleta mabadiliko kwa kuwawezesha Watanzania kupata huduma kwa njia rahisi, salama, na nafuu zaidi. Selcom Pesa imekuja kuondoa changamoto zinazowakabili watumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao, kama vile makato “kasha damu”, ugumu wa kufungua akaunti za benki, usalama na urahisi wa kuzifikia fedha zao wakati wowote.
Katika hafla hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw Emmanuel Tutuba alisisitiza umuhimu wa mapinduzi ya kidigitali ya kifedha nchini Tanzania. Uzinduzi wa Selcom Pesa ni sehemu ya juhudi zinazoendelea kuhamasisha mageuzi ya kiuchumi na kidigitali nchini, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Alieleza jinsi Selcom Pesa inavyowezesha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa makato madogo kuliko ,usalama wa hali ya juu na urahisi wa matumizi hasa katika maeneo yenye upatikanaji mdogo wa huduma za kifedha. Selcom Pesa ni uthibitisho wa uwezo wa sekta binafsi kutumia mifumo hili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kifedha zenye ubora wa hali ya juu na gharama nafuu.
Pia katika hotuba yake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania alieleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika ushirikishwaji wa kifedha, huku kukiwa na ongezeko kubwa la idadi ya wananchi wanaotumia huduma za kifedha kidigitali. Hata hivyo, changamoto ya gharama kubwa za miamala na upatikanaji wa huduma bora za kifedha bado zipo. Selcom Pesa imejidhatiti kushughulikia changamoto hizi kwa kutoa huduma za miamala ya kidigitali kwa gharama ndogo kuliko watoa huduma wengine kama vile benki na mitandao ya simu. Bw Emmanuel Tutuba pia aliwaasa watoa huduma wengine kutumia fursa ya mifumo ya serikali isiyo na gharama kama vile TIPS, ambayo hupunguza gharama za uendeshaji na hivyo kupelekea utoaji wa huduma nafuu kwa wananchi.
Uzinduzi wa Selcom Pesa umeenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya "5 kwa Jero" (Tano Kwa Jero) inayowawezesha wateja kufanya miamala mitano ya ‘Tuma pesa’ na ‘Lipa’ kwa TZS 500 tu kwa siku bila kujali kiwango! Akizungumzia kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Selcom Microfinance, Bw Julius Ruwaichi alisema, Ofa hii ya 5 kwa Jero inawatua wateja wa Selcom Pesa mzigo wa makato makubwa. Ikiwa umejiunga na ofa ya 5 kwa Jero, unaweza kufanya miamala mitano ya tuma pesa na Lipa ya kiasi chochote kwa TSZ 500. Kwa mara ya kwanza nchini Tanzania wateja wanaletwa Bando la Miamala ,ubunifu wa mapinduzi kutoka Selcom Pesa.